} });
 

TANGAZO
RAIS Jakaya Kikwete amesema atahakikisha anamaliza matatizo yote yanayowakabili walimu kote nchini katika kipindi kilichobaki cha utawala wake.
Alitoa ahadi hiyo wakati akizungumza na walimu wapatao 1,500 kutoka wilaya 153 na mikoa yote ya Tanzania Bara, pamoja na wawakilishi kutoka Visiwani.
Akizungumza kwa hisia kali katika eneo la Ngurdoto wilayani Arumeru mkoani hapa katika Mkutano Mkuu wa Tano wa Chama cha Walimu (CWT), Rais Kikwete alisisitiza kuwa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) anachokiongoza, kinaendelea kujali maslahi ya walimu kama watumishi muhimu zaidi katika Taifa.
Alisema kwamba kilio chao ni cha umma na ni wajibu wa viongozi wote kutilia maanani. “Nimeyasikia matatizo yenu kupitia risala maalumu, na mengi tulikwishaanza kuyafanyia kazi.
Nawaahidi kutatua matatizo yenu kabla sijaondoka rasmi mwishoni mwa mwaka huu, na hata kama nitastaafu hapo baadaye, mengine yaliyosalia yataendelea kutatuliwa na viongozi wa serikali ijayo nami binafsi nitaacha maagizo hayo,” alisema Kikwete.
Rais Kikwete aliyeingia madarakani mwaka 2005, anatarajiwa kumaliza muda wake wa uongozi Oktoba mwaka huu, baada ya kuitumikia nchi katika awamu mbili za miaka mitano mitano.
Kikwete pia aliwashauri walimu kuunda chombo kimoja, kitakachowasajili na kuwawakilisha kama Bodi, badala ya hali iliyopo sasa, ambapo kuna utitiri wa vyombo vinavyowawakilisha kiasi cha kusababisha usumbufu wakati mwingine.
Awali, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Taifa (CWT), Yahaya Msulwa alisoma risala ya walimu iliyomuomba Rais Kikwete awatatulie matatizo yao kadhaa kabla hajaondoka rasmi madarakani, kwani mengi ni yale yaliyodumu muda mrefu.
Miongoni mwa madai ya walimu ni pamoja na malimbikizo ya mishahara, posho, malipo ya uhamisho, ucheleweshwaji wa barua za ajira na likizo, na pia maombi yao ya kulipwa posho za muda wa ziada wanaolazimika kuwa kazini.
Wawakilishi kutoka nchi sita pia wako hapa kuhudhuria mkutano huo ambazo ni Uganda, Kenya, Denmark, Rwanda na Ghana, ambapo pia viongozi wastaafu wa CWT taifa na wale wa kutoka visiwa vya Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch alisema chama hicho kimekuwa kikipata ushirikiano mzuri kutoka Serikali ya Awamu ya Nne, na kwamba wanatarajia uhusiano huo mzuri kuendelea hata katika serikali ijayo ya Awamu ya Tano.
Malengo ya mkutano mkuu wa taifa wa CWT ni pamoja na kujadili taarifa za kazi ya chama na taarifa za mapato na matumizi na kupitia mpango mkakati wa miaka mitano 2015-2020.
Uchaguzi mkuu CWT Mkutano mkuu wa CWT leo unatarajiwa kukamilishwa kwa uchaguzi mkuu, ambao umevutia wagombea 28 wa nafasi ya urais wa chama hicho chenye nguvu, kutokana na kuundwa na idadi kubwa ya watumishi wa umma.
Miongoni mwa wagombea hao ni Rais wa sasa wa chama hicho, Gratian Mukoba ambaye pia Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA).
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa hoteli hiyo ya Ngurdoto, huku wajumbe wa mkutano huo na jamii ya walimu kote nchini ikisubiri kwa hamu matokeo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya chama hicho, Kanda ya Ziwa imeongoza kwa kutoa wagombea wengi wakiwemo wa mkoa wa Mwanza ambao ni Kaliyaya Masunga wa Ilemela, Magesa Kirati wa Kwimba, Marwa D. Marwa wa Nyamagana na Mashauri Benedict kutoka Sengerema.
Wengine wa Kanda ya Ziwa ni Charles George wa Geita, Godi Kiduma, Lyangombe Dotto na Malimi Macheyeki kutoka Maswa mkoani Simiyu na Juma Boniface wa Bunda mkoani Mara. Pia yumo Odeka Samson wa Musoma mkoani Mara.
Kutoka Dar es Salaam ni Mukoba wa Ilala, Midelo Mathias wa Kinondoni na Rwebangira Anderson wa Temeke. Kutoka mkoani Pwani ni Maguye Charles.
Mkoa wa Morogoro una wagombea wawili ambao ni Asumbisye Frank na Senyagwa Daudi. Kutoka Dodoma ni Ambakisye Fadhili na Iringa ina mgombea mmoja, Seugali Luth Saida.
Mkoa wa Mbeya umetoa mgombea kutoka Rungwe, Canon Mtewe Leonard. Wagombea wengine ni Christopher Banda kutoka Mtwara na Said Waninga kutoka Lindi.
Mkoa wa Arusha ambao ni mwenyeji wa mkutano huo wa CWT, una mgombea mmoja tu, Laizer Miage kutoka wilayani Karatu. Idadi kama hiyo, yaani wagombea 28, pia wanawania nafasi za Makamu wa Rais na wengi wanatokea mkoa wa Dar es Salaam na Kanda ya Ziwa.
Dar ina wagombea watano na Kanda ya Ziwa wagombea wannne. Wagombea tisa wamejitokeza kuwania ukatibu mkuu na wengi ni kutoka Kanda ya Ziwa ambao ni Fredy Mbuguni, Nyamwero Bwire na Byarugaba Bandiho wote wa Mara, Zacharia Muganda wa Sengerema mkoa wa Mwanza, na Edward Philipo wa Shinyanga.
Wengine ni Elisante Dyamyeku wa Morogoro, Yahya Msulwa wa Kinondoni mkoa wa Dar es Salaam ambaye ni Katibu Mkuu wa sasa wa CWT na Meruma Wasato wa Kibaha mkoani Pwani.
Wanaowania nafasi ya Naibu Katibu Mkuu ni Ezekiel Oluoch na Mpumbe Joseph, wote kutoka Kinondoni Dar es Salaam. Wengine ni Kauka Akyoo na Augustino Daudi kutoka Hai mkoa wa Kilimanjaro, Augustina Massawe wa Moshi Kilimanjaro, na John Gadiye, Anthony Gamba, Mukangara James, na Wilson David, wote kutoka Mwanza.
Pia, wamo Frank Chalamila wa Morogoro, Mayo Wilhelmon wa Manyara, Festo Moshi wa Mbeya, Prosper Mutungi na Tangatya Santuce wa Dodoma, Michael Ndangwe wa Iringa, Shiku Peter na Marwa Mbeu wa Mara.

Wengine ni Abdallah Khalfani na Ismail A. Ismail wa Mtwara. Wengine ni Kanyaiyangiro Evordius, Mathias Midelo na Fidelis Kisukilo kutoka Pwani, Lenda Majebera wa Tabora, Jairos Leonard wa Sumbawanga mkoa wa Rukwa, Raphael Joseph wa Geita na Simu Mussa wa Singida.

soma habar kilasiku kazi ya mikono yangu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 859 030 #ZAMU YAKO 2016

TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top