TANGAZO
Madereva wa daladala, Mussa Kizu (kulia) na Omar Maswa (katikati)
wakizungumza na mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Exuperius Kachenje,
Dar es Salaam jana.
Dar es Salaam. Wakati jana Taifa lilishuhudia mgomo wa madereva wanaodai mambo mbalimbali ikiwamo mikataba ya ajira na mshahara wa Sh250,000 kwa mwezi na kupinga kwenda kwa mara nyingine katika shule ya udereva, imebainika kuwa wengi wao hasa wa daladala, huingiza kati ya Sh900,000 hadi Sh1,050,000 kwa mwezi.
Gazeti hili limebaini kuwa kiasi kama hicho hupata pia makondakta wa mabasi hayo baada ya kugawana walichopata na madereva wao.
Hata hivyo, viwango hivyo hutofautiana kutokana na
njia wanazotoa huduma, aina ya magari wanayoendesha, uamuzi wa dereva,
hata hali ya hewa ya siku husika na idadi ya kukamatwa na askari wa
usalama barabarani.
Uchunguzi unaonyesha kuwa madereva na makondakta
hao kila siku, baada ya kutenga ‘hesabu’ ya tajiri ambayo ni kati ya
Sh100,000 na 150,000, hubakiwa na kati ya Sh80,000 hadi Sh160,000 baada
ya kazi ya siku nzima na hugawana kati ya Sh40,000 hadi Sh80,000 na
kiasi kingine hununulia dizeli kwa ajili ya kufanyia kazi siku
inayofuata. Mabasi mengi yanatumia kati ya Sh60,000 hadi 100,000.
“Inategemea, kwa siku unaweza kupata Sh260,00, au
hata Sh280,000. Kwa mfano, mimi tajiri pesa yake kila siku ni Sh100,000.
Kinachobaki hapo ndicho cha mafuta.
Pia hutegemea aina ya gari, dereva na konda mgawo
wenu hutegemea kinachobaki,” anaeleza dereva wa daladala, Maswa Omari
(38) wa Dar es Salaam. Anaongeza kuwa kwa wastani, kwa siku hubakiwa na
Sh70,000 ambazo hugawana sawa na kondakta wake hivyo kila mmoja
huambulia Sh35,000.
“Lakini fedha hizo ni nje ya kuwalipa ‘deiwaka’.
Unapompa dereva mwenzio ‘deiwaka’ inategemea uhusiano wenu, ingawa kwa
kawaida hulipwa Sh4,000 kwa kila safari,” anasema Omari aliyeeleza kuwa
alianza kazi ya udereva miaka ya 1990.
“Kwa madereva na makondakta wa daladala, chai ni
matumizi nje ya posho, chakula cha mchana, maji, sigara haviingizwi
kwenye hesabu ya siku. Hayo ni matumizi ya kawaida, mtu anaweza kunywa
hata soda tatu kwa siku, akienda hotelini anakula anachotaka kwa gharama
yoyote.
Ndiyo sababu ukiingia kwenye hoteli nyingi za
mjini ni rahisi kumjua kondakta au dereva wa daladala kwani huagiza
tofauti na watu wa kawaida,” anasema Omari.
Dereva mwingine, Njila Shabani anasema fedha
wanazopata kumlipa tajiri na wao kujilipa kwa siku ni nje ya zile
zinazotumika kuwalipa wapiga debe kwenye vituo, kulipia faini kwa askari
wa Kikosi cha Usalama Barabarani (trafiki) pamoja na ile ya kula wake
na kondakta wake.
“Mwanzo wa safari tunawalipa wapiga debe Sh400 kwa
kila safari. Kila kituo tukipakia abiria tunatoa Sh200 au 300 kwa
wapigadebe, hata kwa trafiki kwa siku tunatozwa faini ya Sh30,000 ni
ngumu kukwepa, kama siyo faini halali, basi unaweza kujituka umetumia
hata Sh20,000 kwa siku kutoa kwa askari,” anasema Shabani anayeendesha
gari linalofanya safari zake kati ya Gongo la Mboto na Makumbusho.
Akizungumzia suala la mikataba ya kazi, Omari
anasema wengi wao wana mikataba bandia, waliyotia saini ili kuwawezesha
wamiliki wa daladala kupata vibali vya kuendesha biashara hiyo.
“Ni mikataba hewa kwani ni kwa ajili ya kumsaidia tajiri. Mimi
nina mkataba lakini sijawahi kulipwa mshahara, lakini utafanyaje? Ni
lazima uridhike kwa sababu ndiyo hali halisi,” anasema na kuongeza:
“Kima cha chini cha makubaliano ya mshahara kwenye
mikataba mingi ni Sh150,000 lakini hatupewi, huwezi ‘kusevu’ pesa ,
lakini akili kichwani mwako. Kwa kazi hii isiyo na mshahara, tunaishi
nyumba za kupanga hapa Ilala, vyumba Sh60,000 na watoto wanakwenda shule
kwa ada ya Sh600,000 kwa mwaka.”
Dereva wa daladala ya Buguruni kwenda Makumbusho
kupitia Barabara ya Uhuru, Mussa Kizu anasema anao mkataba na mwajiri
wake. Analipwa Sh250,000 kwa mwezi ingawa wapo madereva wengine ambao
hawalipwi mishahara.
“Matatizo mengi yapo kwa madereva, ingawa ni
waajiri wachache wanaolipa mishahara kwa wakati. Wengi wana mikataba na
mishahara hawapewi,” anasema Kizu mwenye uzoefu wa miaka minne akiwa
dereva wa daladala Dar es Salaam.
Anasema makubaliano yake na mwajiri ni kuwasilisha
Sh100,000 kila siku na kwamba hufanikiwa kubaki na kiasi cha Sh35,000
kwa siku aliyosema inaweza kuzidi au kupungua kutegemea siku.
“Inaweza kutokea ukarudi nyumbani na Sh2,000 au
3,000 kwa kuwa kuna matatizo kadhaa njiani. Kuna trafiki anaweza
kukukamata na kukutoza faini, hapo sasa ni bora kosa liwe la gari bosi
atakuelewa, tatizo umetanua au una makosa ya kutovaa sare, hapo utatoa
fedha na mwishowe hesabu inapungua. Inawabidi fedha ambayo mngegawana na
kondakta wako, iingie kwenye pato la siku la kuwasilisha kwa mwajiri,”
anasema Kizu.
Hata hivyo, anasema trafiki wengi wamekuwa
wakichukua fedha hata mara nne kwa siku kutoka kwao hali inayofanya
waone kazi yao ngumu.
“Wakati mwingine tunakamatwa na kutozwa faini za
hapa na pale. Kwa kawaida kila siku huwa tunatenga Sh20,000 kwa ajili ya
trafiki njiani na hii fedha lazima itumike.”
Kizu mwenye mke na mtoto mmoja, anasema maisha ni
magumu kwa madereva wengi kutokana na kukosekana kwa mikataba
inayowatosheleza, ingawa mwajiri wake humwezesha katika matibabu,
maendeleo na kumuunga mkono anapotaka kufanya jambo kwa ajili ya familia
yake.
“Masilahi madogo na mikataba hewa isiyo na
mishahara, hili ndilo tatizo linalozaa mengine mengi yanayojitokeza kila
siku. Dereva ana mawazo familia yake inakufa njaa,” anasema.
Anasema mgogoro uliopo ambao pia ndiyo sababu ya
mgomo wao siyo wa kushinikizwa, bali waliamua kutokana na suala
lililojitokeza la kutaka warudi darasani kila wanapoomba leseni mpya za
udereva.
“Mgomo wa kwanza ambao ulihusisha mabasi ya
mikoani haukutuhusu, lakini huu wa pili unatuhusu na si kwamba
tumeshinikizwa. Suala la kurudi darasani mwezi mmoja na kulipia
Sh561,000 linanihusu na mimi,” anasema na kutoa wito kwa Serikali kuwa
makini na kutafakari kabla ya kutoa uamuzi ambao huathiri wananchi na
Taifa.
“’Hizi ajali zinazotokea barabarani siyo kwamba madereva wote
wanazisababisha ni wachache ambao wanafanya hivyo kutokana na matatizo
ya kutofuata sheria za barabarani, kama imebainika kwamba dereva
amefanya tatizo apelekwe mahakamani, sheria zifanye kazi na si miswada
ya kila siku wakati tuna Katiba na sheria za kutuongoza.”
Kizu anapendekeza kuwapo kwa semina za mara kwa
mara kwa madereva zitakazochukua muda mfupi, ili kuwawezesha kupata
elimu na pia kujua wajibu wao wawapo barabarani sanjari na kukumbushwa
sheria za barabarani badala ya kurudi darasani kwa siku 30.
Kauli hiyo ya Kizu inaungwa mkono na Omari
anayesema: “Mgomo ni sahihi, ni kweli yanayodaiwa na madereva kuhusu
ajira na mikataba bora ya kazi. Huwezi kutoka Bukoba au Kigoma basi
likiwa na dereva mmoja, hiyo ni hatari, ndiyo sababu wanapiga ‘overtake’
hata kwenye milima au kona kama tulivyoona picha kwenye gazeti la
Mwananchi.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker
Post a Comment