TANGAZO
- LAST UPDATED ON 02 JUNE 2015
- BY MWANDISHI WETU, DODOMA
- HITS: 17
SERIKALI imesisitiza haja ya halmashauri zote nchini kununua tingatinga kupunguza gharama za kutengeneza barabara zake kwa kutumia zabuni hata katika masuala madogo.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje (Chadema).
Katika swali lake la nyongeza, mbunge huyo alisema kwa kutambua gharama za matengenezo ya barabara, serikali haioni kama inafaa kutoa amri ya kununua tingatinga.
Majaliwa alisema kwamba serikali ilishawahi kushauri halmashauri kuona umuhimu wa kununua tingatinga, kutengeneza barabara zake na kumtaka Wenje kushawishi baraza la madiwani kuona umuhimu huo ili kupunguza gharama.
Swali la nyongeza la Wenje limetokana na swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Annamerystella Mallac (Chadema) aliyetaka kujua lini serikali itatenga fedha za kutengeneza mitaro kuokoa fedha zinazotumika mara kwa mara kutengeneza barabara zinaposombwa na maji.
Alikuwa akizungumzia barabara za halmashauri za miji na wilaya, ikiwemo Mpanda na Sumbawanga, ambao huharibika mara kwa mara kwa ukosefu wa mitaro.
Majaliwa alisema kwamba serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mitaro katika barabara za mijini na katika halmashauri ya mji wa Mpanda kuanzia mwaka wa fedha 2012/2013 hadi 2014/2015 jumla ya shilingi milioni 502 zimetumika kujenga mitaro ya maji ya mvua.
Aidha, alisema kwamba kwa sasa mji wa Mpanda una kilomita 20.2 za mitaro ya maji ya mvua wakati zinahitajika kilomita 251 za mitaro ya maji.
Aidha, ili kuendeleza ujenzi huo katika bajeti ya mwaka 2015/2016, zimeombwa Sh milioni 150 za kuendeleza ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua katika barabara za mji wa Mpanda.
Akizungumzia halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga, yenye jumla ya kilometa 204.55 za mtandao wa barabara za mjini, kunahitajika kilometa 409.10 za mitaro ya maji ya mvua.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker
Post a Comment