TANGAZO
11th June 2015
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amewataka viongozi kuacha kuwapa vitisho wananchi wanaojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura hali itakayowafanya wakose haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowahitaji.
Kinana alitoa onyo hilo baada ya kupokea malalamiko ya baadhi ya wananchi wilaya ya Bukoba na Muleba ya kuelezwa na viongozi na watendaji wa serikali kuwa siku za kujiandikisha ni mbili badala ya saba zilizotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kinana alisema hakuna sheria na kanuni kama hizo zilitolewa na serikali za kupunguza siku za kujiandikisha kwa baadhi ya maeneo nchini na kuwataka viongozi kumaliza tatizo hilo mara moja.
“Jambo kama hilo halipo na huyo aliyewatajia siku za kujiandikisha ni mbili, anahitaji kuchukuliwa hatua za kisheria, haiwezekani awatajie siku alizoamua yeye huku ni kuwanyima haki ya msingi ya Watanzania wenye sifa za kujiandikisha kupata haki yao ya kupiga kura na kuchagua kiongozi wanayemuhitaji,” alisema Kinana.
Wananchi hao walimueleza Kinana kuwa watendaji hao waliwaeleza kuwa siku za kujiandikisha ni mbili badala ya saba, hali ambayo iliwafanya wapatwe na hofu ya kukosa kujiandikisha na kupiga kura.
Kufuatia malalamiko hayo Kinana, alimuagiza Mkuu wa mkoa wa Kagera, John Mongella, kukahakikisha jambo hilo linapatiwa ufumbuzi haraka.
Mongella alisema alishapata taarifa kuhusu jambo hilo na alishaanza kulifanyia kazi na kwamba alielezwa kuwa sababu za kufupisha siku ni wananchi wawahi kwenye vituo kujiandikisha.
“Nimeshalifanyia kazi na nilihoji nikaambiwa eti walikuwa wanawadanganya wananchi ili wajitokeze kwa wingi na haraka siku za mwanzo. Nimeshaongea nao na nimewaeleza marufuku kurudia tena kosa hilo na wananchi watajiandikisha kwa siku zilizopangwa saba,” alisema Mongella.
Kinana aliwataka viongozi wa mkoa, wilaya, vijiji na vitongoji kuhakikisha wananchi wenye sifa za kujiandikisha wanafanya hivyo.
Aliwaambia wananchi hao wajiandikishe kwenye daftari la wapigakura kwani licha ya kupiga kura, pia ni kitambulisho muhimu kinachoweza kuwatambulisha mahali popote.
CHANZO: NIPASHE
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker
Post a Comment