TANGAZO
| Spika wa Bunge, Anna Makinda. |
KATIKA jitihada za kuhakikisha wabunge wa CCM na wachache wa upinzani walioko bungeni wanamsikiliza Rais Jakaya Kikwete akihutubia Bunge leo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai amelazimika kuliahirisha hadi leo asubuhi kujadili suala la kiinua mgongo chao.
Huku ikielezwa kuwa kuna uwezekano wabunge hao wasihudhurie mkutano wa Rais, endapo hawataelezwa jambo linaloeleweka kuhusu fedha hizo, habari zingine za kuaminika kutoka ndani ya bunge hilo zinasema lengo lao ni kushawishi kusitishwa kuvunjwa kwa bunge ili jambo hilo litafutiwe ufumbuzi.
Kuna madai kuwa kiwango cha kiinua mgongo cha zaidi ya Sh milioni 230 kimepunguzwa hadi Sh milioni 160 kwa kila mbunge na kuwa, tofauti na walivyoelekezwa na Spika Anne Makinda kuwa wangekuta fedha zao hizo kwenye akaunti zao za benki, hakuna walichokikuta na hawajui watakikuta lini wala kiasi halisi.
Akiahirisha Bunge jana jioni kutokana na ombi la mwongozo lililotolewa na Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa, aliyesimama kukumbushia mwongozo wa Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangala uliotolewa asubuhi na kuahidiwa kutolewa majibu muda huo, Ndugai alisema, majibu sahihi yangeletwa bungeni hapo baadaye.
Kwa mujibu wa Ndugai, tayari Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Bunge ilikuwa imekutana kujadili suala hilo, ambalo hata hivyo hakulitaja wazi, hivyo, wabunge wangekuwa wametenda vema kuendelea kujadili Muswada wa Sheria ya Kuunda Tume ya Walimu ya Mwaka 2015.
Hata hivyo, baada ya kusema hivyo, wabunge walionesha kutoridhishwa na kuendelea kudai majibu wakati huo, kwa maelezo kuwa akili zao zilikuwa mbali, na walihitaji kuelezwa kinachoendelea kuhusu walicho kiita bungeni hapo kuwa ni ‘maslahi ya walimu’ ili saikolojia yao ikae sawa na kurejea kwenye shughuli za Bunge.
“Mheshimiwa Naibu Spika, tumewajibika kwenye Bunge hili kwa uaminifu wa hali ya juu, na tuliambiwa na Spika kuwa kila kitu kitakuwa sawa. Sasa muswada huu ni wa muhimu sana wa walimu inabidi akili zetu ziwe sawa ili tujadili vifungu sawa sawa”.
“Kama alivyoeleza Dk Kigwangala asubuhi, tunasikia tu tetesi zikizunguka (hakusema ni za nini) na kesho (leo) ndio bunge linavunjwa na Rais Jakaya Kikwete, tunaomba tusichukulie suala hili kuwa ni dogo, Bunge liahirishwe hadi kesho ili tukalijadili yanayotakiwa akili zetu zikiwa zimetulia,” Ndasa alisema.
Baada ya kueleza hayo, Naibu Spika alisema, “Naahirisha bunge hadi kesho saa tatu asubuhi.”
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker
Post a Comment