} });
 

TANGAZO

Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba
HATIMAYE baada ya hujuma ya wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani kushindwa, Serikali imewasilisha bungeni miswada ya sheria kuhusu masuala ya mafuta na gesi, huku matumizi ya mapato ya gesi yakiwekewa vizingiti.
Akisoma hotuba ya Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015 bungeni jana, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema muswada unaweka masharti kuhusu uanzishwaji wa Mfuko wa Mafuta na Gesi, ambao utakuwa na akaunti mbili zitakazotunzwa na kusimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Alizitaja akaunti hizo ni Akaunti ya Kupokea Mapato na Akaunti ya Kutunza Mapato na kwamba mfuko wa mapato yatokanayo na mafuta na gesi, unapendekezwa kuanzishwa kwa madhumuni ya kupokea na kugawa mapato yatokanayo na mafuta na gesi kwa kuzingatia malengo makubwa matatu.
Malengo, mapato
Malengo hayo ni kuhakikisha uimara wa kifedha na kiuchumi, kugharamia uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi, kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kulinda rasilimali kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Katika muswada huo, Nchemba pia alitaja vyanzo vya mapato vya mfuko huo kuwa ni mirabaha, gawio na faida ya Serikali katika shughuli za mafuta na gesi.
Vingine ni kodi za mapato ya makampuni, ambayo hukatwa baada ya kupata faida ghafi na gawio litokanalo na tasnia ya mafuta na gesi pamoja na faida itakayopatikana kutokana na uwekezaji wa fedha za mfuko.
Mwenendo wa akaunti
Nchemba alisema inapendekezwa katika muswada kwamba mapato yote ya mfuko yawekwe kwenye Akaunti ya Kupokea Mapato.
Baadaye, Akaunti ya Kutunza Mapato itapokea kiasi cha asilimia ya mapato kutoka kwenye Akaunti ya Kupokea Mapato kwa kuzingatia miongozo ya kibajeti.
Kizingiti
Naibu Waziri Nchemba alisema muswada pia unaweka zuio kwenye matumizi ya mapato ya mfuko ambapo mapato hayo hayatatumika kwa ajili ya kutoa mkopo kwa Serikali, taasisi za umma, taasisi za sekta binafsi au kwa mtu au taasisi yoyote.
Alisema muswada pia unapendekeza masharti yanayoweka miongozo ya kibajeti ambayo itakuwa ni msingi wa mgawanyo wa mapato kutoka kwenye mfuko.
“Vilevile, sehemu hii inapendekeza kuanzisha Bodi ya Ushauri wa Uwekezaji kwa lengo la kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha kuhusu mikakati ya kiuwekezaji ya Akaunti ya Kutunza Mapato ya Mfuko,” alisema.
Alieleza kuwa Bodi hiyo itakuwa na wajibu wa kumshauri Waziri kuhusu masuala yote ya uendeshaji wa Akaunti ya Kutunza Mapato, kufanya utafiti na kuandaa miongozo ya uwekezaji wa kimkakati, na kupendekeza kwa Waziri sera za uwekezaji.
“Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi watateuliwa na Rais. Aidha, masuala yanayohusu Sekretarieti ya Bodi na Usimamizi wa Mfuko pia yameainishwa katika sehemu hii,” alisema.
Alieleza kuwa muswada huo unahusu miongozo ya kibajeti kwa lengo la kutoa miongozo kuhusu ugharamiaji wa bajeti ya Serikali, Kampuni ya Taifa ya Mafuta, ustahimilivu wa kifedha na utunzaji wa fedha kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Petroli wa Mwaka 2015, alisema unalenga kuondoa changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye sera, sheria na miongozo mbalimbali ambayo ilikuwepo kwa muda mrefu ili kuleta ufanisi bora zaidi katika sekta ya gesi asilia.
Ushiriki wa Watanzania
Alisema hatua hiyo ni kutoa fursa kwa Watanzania kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kiuwekezaji katika sekta za mafuta na gesi asilia nchini.
Simbachawene alisema pia muswada huo utaanzisha mfumo imara wa kisheria, kiutawala na kimenejimenti kuhusu usimamizi na udhibiti wa shughuli zote za mafuta na gesi nchini.
Alisema muswada huo unaanzisha taasisi tatu mpya ambazo ni Ofisi ya Ushauri Kuhusu Petroli na Gesi chini ya Ofisi ya Rais, Kampuni ya Mafuta ya Taifa na Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (PURA).
Akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uchimbaji Tanzania wa Mwaka 2015, Waziri Simbachawene alisema muswada huo unaweka uwazi katika leseni na mikataba ya madini, gesi na mafuta.
Alisema muswada ukipitishwa utafanya mikataba yote ya madini na gesi iwe wazi na halitakuwa j ambo la siri kama ilivyo sasa.
Pia alisema ushiriki wa Watanzania lazima uwe wazi ijulikane wameshiriki kwa kiasi gani tofauti na sasa na kwamba pia gharama za uwekezaji na uzalishaji nazo zinatakiwa kuwa wazi, mambo ambayo ndiyo sababu wanataka yaharakishe miswada hiyo.
Alisema sheria italazimisha kujua taarifa kuhusu uwekezaji kama ni halisi na sahihi na kwamba hilo ni jambo muhimu na ndiyo sababu wanataka uwazi uwe katika sheria.

soma habar kilasiku kazi ya mikono yangu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 859 030 #ZAMU YAKO 2016

TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top