} });
 

TANGAZO
KIKAO cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara juzi kilivunjika baada ya madiwani hao kudai kuwa maazimio ya vikao vilivyopita kushindwa kutekelezwa bila ya sababu za msingi.
Kikao hicho kilichokuwa na ajenda tano kilianza kwa ajenda namba moja ya kufungua kikao lakini ghafla zikarukwa ajenda nyingine na kusomwa ajenda ya kupitia muhtasari wa vikao vilivyopita vya baraza hilo.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Peter Tendee ndiye aliyeanza kwa kusema kuwa haina haja ya kuendelea na kikao hiki cha baraza kwa kuwa maazimio ya vikao vilivyopita kushindwa kutekelezwa na Mkurugenzi, Grace Mbaruku.
Tendee alisema moja ya maazimio ya kamati ya fedha, uongozi na mipango ni pamoja na kumtaka Mkurugenzi Mbaruku kumrudisha kazini Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Happy Fungo.
Baada ya kauli hiyo ya Mwenyekiti ambayo iliungwa mkono na karibu madiwani wote ilipitishwa kuwa haina haja ya kuendelea na kikao hicho kwani Mkurugenzi huyo amewadharau na hawataki kufanya naye kazi tena.
“Nyie wananchi nataka msikie kuwa sisi madiwani hatumtaki huyu Mkurugenzi kwani hatekelezi maazimio ya vikao na pili yeye pia ni mbadhirifu,” alisema Tendee.
Baada ya kauli hiyo ghafla madiwani wote walisimama na kutoka nje ya ukumbi na kuendelea na shughuli nyingine na kuwaacha watendaji wa halmashauri hiyo wasijue la kufanya kutokana na maamuzi hayo.
Akizungumza kwa njia ya simu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Simanjiro, Grace Mbaruku alisema kuwa mwanasheria wa halmashauri hiyo, Fungo aliyesimamishwa kazi tangu mwaka jana hana sifa za kuiongoza halmashauri hiyo.
Alisema maazimio ya kamati ya fedha, uongozi na mipango ilipelekwa kwenye baraza la madiwani la kikao kilichopita kilichohudhuriwa na wataalamu wa Tamisemi Mkoa wa Manyara ambao waliwaeleza madiwani hao kuwa hawana mamlaka ya kumlazimisha Mkurugenzi huyo kumrudisha kazini mwanasheria huyo.
Mbaruku alisema hatua aliyochukua ya kumsimamisha Fungo ulizingatia taratibu, kanuni na sheria za kazi na yeye ndiye mwenye mamlaka ya kumchukulia hatua mtumishi yeyote wa halmashauri hiyo na sio mtu mwingine.
Alisema Fungo hana sifa za kuwa mwanasheria kwani amekuwa akipotosha madiwani katika vikao mbalimbali kwa kutafsiri sheria isiyokuwepo kwa maslahi ya wanasiasa hao na sio kwa ajili ya halmashauri hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa baada ya kuona hali hiyo alifanya kazi ya ziada ya kutaka kujua uhalali wa vyeti vyake na aligundua mambo mengi sana.

soma habar kilasiku kazi ya mikono yangu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 859 030 #ZAMU YAKO 2016

TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top