TANGAZO
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imeanzisha utaratibu mpya wa mafunzo kwa vitendo kwa watendaji wanaoandikisha wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR).
Jumla ya BVR kits 498 zitatumika kutoa mafunzo hayo, lengo likiwa ni kurahisisha uandikishaji, baada ya awamu ya kwanza kusuasua katika Mkoa wa Njombe.
Mafunzo hayo yatafanyika kwa mikoa minne ya awamu ya tatu ya uandikishaji wapiga kura na yatakuwa endelevu ili kuharakisha uandikishaji utakaoanza Mei 2, mwaka huu. Mkurugenzi wa Nec, Julius Malaba, akizungumza na NIPASHE jana kwa njia ya simu, alisema Nec imeamua vifaa hivyo vitumike kwenye mafunzo ya vitendo kwa watumishi hao ili kuharakisha uandikishaji.
Awamu ya kwanza ya uandikishaji ilikuwa Mkoa wa Njombe, ya pili inayoanza kesho ni Mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa na awamu ya tatu ni Dodoma, Mbeya, Katavi na Tabora.
“Tumeamua BVR kits zilizotumika mkoani Njombe 250 na 248 zilizowasili mwanzoni mwa Aprili, mwaka huu, zitatumika kwa mafunzo ili tunapofika kwenye uandikishaji uende haraka zaidi,” alisema. Mikoa ya awamu ya pili ya uandikishaji kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 kwa Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, ina jumla ya watu wenye sifa ya kupiga kura ifikapo Oktoba, mwaka huu wapatao 4,306,569.
Malaba alisema BVR 1,600 zilizowasili katikati ya Aprili, mwaka huu, zitatumika kuandikisha katika mikoa ya Iringa, Lindi, Mtwara na Ruvuma yenye watu wenye sifa ya kupiga kura ifikapo Oktoba, mwaka huu ni 2,599,205.
Tangu Februari 23, mwaka huu, Nec ilianza uandikishaji katika Mkoa wa Njombe wenye watu wenye sifa za kupiga kura 392,634, lakini hadi uandikishaji unafika Aprili 18, mwaka huu, walikuwa wameandikishwa watu 300,080 ikiwa ni tofauti ya watu 92,554.
Mkurugenzi huyo alisema BVR 1,600 zitakazowasili kati ya Jumamosi na Jumapili wiki hii, zitatumika kwenye awamu ya pili ya uandikishaji wapiga kura.
Alisema kwa sasa mafunzo kwa vitendo kwa idadi ya BVR zilizopo ni endelevu ili wakati wa uandikishaji kusiwe na ucheleweshaji kama ilivyotokea kwenye Mkoa wa Njombe kutokana na ugeni wa matumizi ya mashine hizo.
Aprili 2, mwaka huu, Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alitangaza kuahirishwa kwa Kura ya Maoni kwa Katiba inayopendekezwa kutokana na kushindwa kukamilika kwa daftari la kudumu la wapiga kura na itatangazwa tena.
Alisema tarehe ya kura hiyo itatangazwa tena baada ya Nec kushauriana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec).
Nec ilisema hadi wakati huo, serikali ilikuwa imetoa Dola milioni 72 za Marekani (sawa na Sh. bilioni 13).
Vifaa hivyo vinanunuliwa na serikali kupitia kampuni ya Lithotech Export ya Afrika Kusini ambayo imeingia mkataba na Nec na inaviagiza China.
Taarifa zilizopatikana ndani ya tume hiyo zinaeleza kuwa, kampuni hiyo ndiyo inayotoa muundo wa ndani (soft ware) ya mashine hizo na kwamba utengenezaji wa mashine moja na kuweka vifaa vyote muhimu inachukua wiki sita.
Hadi sasa Nec imeshapokea BVR kits 2,098 na zilizokuwa zimeagizwa kukamilisha uandikishaji nchi nzima ni 8,000.
Nec ilieleza kuwa matarajio yake ni kuwa ifikapo Julai mwaka huu, uandikishaji ukamilike nchi nzima.
Pia uandikishaji utaendelea kwenye mikoa yote na Jiji la Dar es Salaam na Zanzibar itakuwa ya mwisho ili BVR kits zote zitumike kwa pamoja kwenye mikoa hiyo.
CHANZO: NIPASHE
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker
Post a Comment