TANGAZO
Winga wa Yanga ya jijini Dar es Salaam, Mrisho Ngasa, amesema kwamba licha ya hali ya machafuko inayoendelea nchini Afrika Kusini ya wazawa dhidi ya wageni, hatasita kwenda huko endapo atapokea mwaliko wa kujiunga na klabu yoyote itakayomuhitaji.
Ngasa ambaye alirejea Yanga akitokea Simba kwa mkopo, anatarajia kumaliza mkataba wake Jangwani mwezi ujao.
Ngasa ambaye mwaka jana alikwenda Afrika Kusini kufanya majaribio 'kinyemela', anatajwa kuwa kwenye mipango ya kuhamia Free State Stars ya huko na ndio inayofanya achelewe kusaini mkataba mpya na Yanga.
Akizungumza na NIPASHE jana jijini, Ngasa alisema kwamba yeye ni mchezaji na yuko tayari kwenda Afrika Kusini kujiunga na timu yoyote itakayoridhishwa na kiwango chake.
Mshambuliaji huyo ambaye juzi alifunga goli moja katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Stand United, alisema kwamba soka ndio ajira yake hivyo anaamini kwamba akipata nafasi ya kwenda Afrika Kusini au nchi nyingine atakwenda kucheza mpira sehemu iliyo salama kwa sababu hatakuwa peke yake uwanjani.
"Mimi ni mwanajeshi, nitakwenda vitani wala sitaiachia fursa hiyo ikitokea, kiukweli wala sitahofia," alisema mshambuliaji huyo.
Alisema kwamba bado anaamini ana nafasi ya kwenda kucheza soka nje ya nchi na pia kuitumikia timu ya taifa (Taifa Stars) kwa muda mrefu.
Nyota huyo sasa amekuwa na ndoto za kucheza soka la kulipwa tofauti na mwaka 2012 alipokataa ofa ya kujiunga na El Merreikh ya Sudan iliyomuhitaji wakati huo akiwa anaichezea Azam.
Kutokana na Ngasa kukataa ofa ya El Merreikh na kuonyesha mapenzi yake kwa Yanga kwa kuibusu nembo ya klabu hiyo, Azam ilimtoa kwa mkopo Simba ambako aliitumikia kwa msimu mmoja.
Mbali na Ngasa, mchezaji mwingine wa Yanga aliye katika kikosi cha kwanza ambaye anamaliza mkataba mwezi ujao ni Mnyarwanda Haruna Niyonzima.
CHANZO: NIPASHE
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker
Post a Comment