TANGAZO
| Add caption |
WAKULIMA wa zao la kahawa wilayani Mbinga wameanza kunufaika na huduma za bima ya afya kutoka Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Wakulima hao waliotembelea makao makuu ya mfuko huo wa hifadhi ya jamii jijini Dar es Salaam jana, walitoa shukrani zao kwa uongozi wa shirika hilo kwa ushirikiano inaouonesha kwao.
Mwaka jana wakulima katika wilaya hiyo kupitia vyama vya msingi vya ushirika vilifaidika na mkopo kutoka NSSF wenye thamani ya Sh bilioni 2 walioutumia kununulia zao hilo.
Katika ziara hiyo, ujumbe wa wakulima wanane uliwakilisha wenzao na kuongozwa na Mbunge wa Mbinga Magharibi, Gaudens Kayombo.
“Wakulima wetu wa zao la kahawa wamejiunga na shirika hili na wamekuwa wanachama na sasa wameanza kupata bima ya afya...ni jambo la kujivunia na la mafanikio,” alisema.
Alisema hii ni mara ya kwanza kwa wakulima wadogo kuanza kupata bima ya afya ambapo wanatibiwa pamoja na familia zao kwa uhakika zaidi.
“Kutokana na manufaa haya, wakulima hawa wamekuja Dar es Salaam kuwashukuru viongozi wa shirika la NSSF na kuimarisha zaidi mahusiano yaliyoanza kuota mizizi,” alisema.
Vyama vilivyopata mkopo huo na kununua mazao kutoka kwa wakulima ni pamoja na Ngaka Amcos, Pilikano Amcos, Mahilo Amcos na Ngima Amcos.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, mkopo huo umewezesha familia kupeleka watoto wote waliofaulu kidato cha saba mwaka huu kwenda sekondari ikilinganishwa na asilimia 50 tu walioweza kujiunga na masomo hayo mwaka jana.
“Wamekuja tena kuomba mkopo kwa ajili ya msimu huu na kuna vyama vingine 12 vimeongezeka pamoja na vile vinne vya awali,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi wa mfuko huo, Yacoub Kidula alisema vyama hivyo vya msingi vinastahili sifa kwa vile viliweza kurudisha mkopo ndani ya siku 100 badala ya miaka miwili kama mkataba ulivyowataka awali.
“Kutokana na utendaji wao na uaminifu wao katika mkopo huu, msimu huu tunawakaribisha waje wakope tena,” alisema. Aliwashauri pia kulenga katika kuongeza uzalishaji, kukoboa na kusindika zao hilo mbali na kununua tu. .
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker
Post a Comment