} });
 

TANGAZO



Mnikulu Shabani Gurumo
Mnikulu  Shabani Gurumo, aliyepokea asante ya Shilingi milioni 80.8 katika mgawo wa  fedha za kashfa ya   akaunti ya  Tegeta Escrow, ametimuliwa kazi  Ikulu.

Taarifa za kuondolewa Gurumo, zilitolewa na Katibu Mkuu  Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue , katika mahojiano na gazeti hili ambaye alisema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa wiki moja iliyopita.

Gurumo aliyekuwa na wadhifa wa Ofisa Mkuu wa  Ikulu, alikiri kupokea fedha hizo  kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing  James Rugemalira, alipohojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.

Rugemalira alikuwa mbia (mzawa) wa kampuni binafsi ya kuzalisha umeme ya IPTL ambayo pamoja na Tanesco zilifungua akaunti hiyo ya Escrow.

Fedha alizopokea Gurumo zinadaiwa kuwa ni sehemu ya zaidi ya Shilingi  bilioni 300 zilizochotwa kifisadi katika akaunti hiyo, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Balozi Ombeni alisema hawana cha kumfanya kwa upande wao na kwamba Ofisi ya Utumishi wa Umma ndiyo yenye jukumu la kuamua kinachofuata dhidi ya mtumishi huyo.  “Sisi hatuna cha kufanya zaidi ya kuondolewa Ikulu,  Ofisi ya Utumishi itaamua nini kinachofuata.”

Awali Mnikulu huyo alipinga madai ya yeye kupewa zawadi hiyo ya Escrow na lakini alikiri kuwa alipokea Shilingi  milioni 80.8 kutoka kwa  Rugemalira kwa sababu za  urafiki walionao kwa muda wa miaka 10 na hazihusiani na mgawo.

Gurumo alieleza kuwa  Rugemalira ni rafiki yake kwa muongo mzima na kwamba  ndiye aliyemshauri kufungua akaunti kwenye Benki ya Biashara ya Mkombozi, tawi la St. Joseph, jijini Dar es Salaam, kabla ya kumuingizia kiasi cha Shilingi  80, 850,000 katika akaunti hiyo.

Aliwaambia wajumbe wa Tume ya Maadili kuwa  aliyemuunganisha na Rugemalira, ni Dk. Fred Limbanga wa hospitali binafsi ya Sanitas, iliyoko Mikocheni, Dar es Salaam.

Alijieleza zaidi kuwa  hata siku moja hajawahi kuwa na maslahi ya kiuchumi na Rugemalira, mbali na ya kifedha na pia hana uhusiano wowote na kampuni ya VIP Engineering and Marketing.

Akasema anahisi pengine Rugemalira alifanya hivyo kwa kuwa kipindi hicho alikuwa ana mgonjwa anayesumbuliwa na maradhi ya saratani.

 Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ilitoa taarifa kuwa Shilingi bilioni 301 zilichotwa kwenye akaunti hiyo na kusababisha vigogo kadhaa akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema kujiuzulu.

Wengine waliopokea mgawo ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alikiri kupokea  shilingi bilioni 1.6, ambazo zilisababishwa  kutimuliwa uwaziri.

Pamoja naye Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, naye akijiuzulu kwa kashfa hiyo iliyosimamiwa na wizara yake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombane, alipoulizwa kuhusu kutimuliwa kwa kiongozi huyo na hatua gani zitakazochukuliwa alilitaka gazeti liwasiliane na Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo,  Hab Mkwizu kwa ufafanuzi.

Hata hivyo, hakupatikana hadi gazeti hili lilipokwenda mitamboni.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

soma habar kilasiku kazi ya mikono yangu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 859 030 #ZAMU YAKO 2016

TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top