TANGAZO
> Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba akionyesha begi lenye fomu za kuomba kugombea kiti cha Urais wa kupitia chama cha CCM baada ya kukabidhiwa makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Na Fidelis Butahe
Makada wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mwiguli Nchemba na Godwin Mwapongo, jana waliongeza idadi ya wanaCCM wanaotaka kuwania urais, baada ya kufika makao makuu ya chama hicho tawala mjini Dodoma na kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo ya juu serikalini.
Wakati Mwigulu ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha akifika ofisini hapo majira ya saa 4:00 asubuhi, Mwapongo ambaye ni Wakili Mwandamizi katika Mahakama Kuu ya Tanzania alifika majira ya saa 6:00 mchana.
Nchemba atembea kwa miguu
Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi, jana alitembea kwa miguu kutoka bungeni hadi Ofisi za Makao Makuu ya CCM kuchukua fomu za kuwania urais.
Hatua hiyo imesababisha wananchi kupigana vikumbo katika maeneo aliyopita wakitaka kumshika mkono, huku baadhi wakimsindikiza hadi katika ofisi hizo.
Akiwa ameongozana na mkewe, mara kwa mara Mwigulu alikuwa akiwapungia mkono wananchi hao na wao kumjibu kwa kumpigia makofi na kuimba ‘rais, rais’.
Tofauti na wagombea wengine waliochukua fomu, Mwigulu alitaja mali zake na kiwango cha fedha alichonacho katika akaunti yake Benki, huku akisema kuwa mpaka sasa hajui kuendesha gari.
Wabunge walioambatana na Mwigulu ni Margaret Sitta, Martha Mlata, Mary Chatanda (wote Viti maalum), Modestus Kilufi (Mbarali) na Mohamed Missanga (Singida Magharibi).
Margaret ambaye mumewe, Samuel Sitta naye ametangaza nia ya kugombea urais alipoulizwa sababu za kumuunga mkono Mwigulu alisema, “Napenda kusikiliza kauli za wagombea urais wote wa CCM ili kujua kila mmoja ana mpango gani wa kuisaidia nchi yetu.”
Ataja utajiri wake
Katika mkutano wake na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu, Mwigulu alieleza mali alizonazo kuwa ni nyumba mbili na Sh5milioni zilizopo Benki, huku akifafanua kuwa nyumba ya tatu amewajengea wazazi wake, hivyo hawezi kusema kuwa ni yake.
“Kwa sasa ndiyo nipo katika hatua za mwisho za kumalizia kujenga nyumba yangu kijijini, juzi tu hapa nimekopa pato langu la mwisho la ubunge,” alisema.
Alisema kwa muda mrefu amekuwa akitumia gari la CCM na wakati mwingine kupewa lifti na mkewe, na kufafanua kuwa kabla na baada ya kuwa mbunge hakuwahi kujifunza kuendesha gari.
“Nilipokuwa mbunge na baadaye waziri nilipewa gari la kutumia na serikali na chama. Sasa naelekea kuwa rais nitapewa gari, hivyo sidhani kama nitajifunza kuendesha gari,” alisema.
“Katika akaunti yangu nina Sh5milioni. Siku za hivi karibuni rafiki yangu Nasoro amenipa gari ili nilitumie katika shughuli hii niliyoianza. Kwa sasa sina gari la chama kwa sababu nimeshalirejesha na pia siwezi kutumia gari ya serikali kuzunguka nchi nzima,” alisema Mwigulu ambaye aliondoka katika ofisi hizo na gari lenye namba za usajili za STK.
Aliongeza, “Utajiri mkubwa wa mtu uko mioyoni mwa Watanzania. Ile nyumba yangu ya Dar es Salaam niliijenga baada ya kuchukua mkopo wakati nikifanya kazi Benki Kuu ya Tanzania.”
Mwigulu alisema Mwalimu Julius Nyerere anaitwa Baba wa Taifa kwa sababu watoto wote wa Tanzania aliwaona kama watoto wake, kufafanua kuwa hata yeye ana mapenzi makubwa kwa Watanzania.
Azungumzia utaratibu wa bajeti za wizara kutenga fedha za chai alisema, “Watu watakunywa chai watakapotoka nyumbani, mbona anayekwenda kuchunga mifugo hatengewi chai? Hatutaweza kutenga fedha nyingi kwa matumizi yanayowanufaisha wachache na kuacha mambo ya msingi.”
Kuhusu kukua kwa deni la taifa alisema, “Deni hili limekuwa katika serikali ya awamu ya nne. Watu hawajui tu ila ukweli ni kwamba hivi sasa kuna miradi zaidi ya 280 ambayo utekelezaji wake unafanyika kwa fedha za mkopo. Hii miradi ya ujenzi wa bomba la gesi, viwanja vya ndege na Chuo Kikuu Dodoma pamoja na barabara inafanyika kwa fedha hizo.”Alisema mradi wa gesi ukikamilika utapunguza gharama za uzalishaji na kufafanua kuwa jambo hilo litakuza uchumi wa nchi.
“Sasa tujiulize nini bora, kuwa na deni dogo la taifa harafu maendeleo hakuna au tuwe na deni, lakini tunafanya mambo ya msingi. Kwa mazingira tuliyokuwa nayo mikopo hii niliyoieleza ilikuwa haikwepeki,” alifafanua.
Alisema kutokana na juhudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne, rais wa awamu hiyo ndiyo atakuwa wa mwisho kuiongoza Tanzania masikini.
“Tunatafuta rais mtanzania, anayeyajua maisha ya watanzania na aliyebeba ajenda zao. Uongozi katika taifa letu ni sawa na kujenga nyumba, kuna anayejenga msingi, kuta, anayemalizia ujenzi (finishing). Tumeshavuka awamu nyingi na kila awamu kuna kazi imefanya,” alisema.
Waulizeni maswali magumu
Mbali na Mwigulu, kada mwingine wa chama hicho aliyechukua fomu jana ni Godwin Mwapongo ambaye ni wakili mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Mwapongo aligoma kuzungumza kwa kina juu ya nia yake hiyo, huku akisisitiza kuwa atazungumza kwa kirefu na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kesho.
Akizungumza kwa kifupi, Mwapongo aliwataka Watanzania wanaodhani kuwa wanaweza kuwania urais wajitokeze ili wapate fursa ya kuwatumikia Watanzania wenzao.
Huku akisisitiza kuwa atazungumza zaidi kesho katika mkutano wake na wanahabari, aliwataka waandishi wa habari kuwauliza maswali magumu wagombea urais.
“Mtu anasema atajenga viwanda…, huyo mnatakiwa kumuuliza maswali magumu maana hata tukikusanya kodi asilimia 100 hatuwezi kujiendesha sisi wenyewe. Hivi viwanda atavijenga vipi na atafanya nini cha ziada. Mkituuliza maswali magumu wananchi watatupambanua kwa yale tunayoyasema,” alisema.
Watakaochukua Fomu
Watakaochukua fomu za kugombea urais leo Jumapili ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Peter Nyalali
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker
Post a Comment