TANGAZO
KLABU ya Simba imesema itamchukulia hatua za kisheria mchezaji wao Ramadhan Singano kwa kuidhalilisha na kupotosha umma kuhusu mkataba wake.
Kwa zaidi ya wiki mbili sasa kumekuwa na mvutano kati ya klabu na Singano kuhusu mkataba ambapo mchezaji huyo anasema amemaliza mkataba wake wa miaka miwili na uongozi wa Simba ukisema bado mchezaji wake halali kwa vile walisaini naye mkataba wa miaka mitatu unaotarajiwa kumalizika mwakani.
Makamu wa Rais wa Simba Geofrey Nyange ‘Kaburu’ aliliambia gazeti hili jana kuwa Singano anapotosha umma kuhusu ukweli wa mkataba wake huku akimwonesha mwandishi wa gazeti hili nakala za mkataba huo.
Kwa mujibu wa vielelezo vilivyoonyeshwa na Nyange, Singano alisaini mkataba wa miaka mitatu unaotakiwa kumalizika Julai.
Aidha, ndani ya mkataba huo kuna saini ya Singano ya maandishi na kidole gumba, saini ya Makamu wa Rais aliyepita Joseph Itang’are ‘Kinesi’ na aliyekuwa Katibu Mkuu ambaye pia ni mwanasheria Evodius Mtawala.
Alisema ili kutafuta ukweli wa mkataba wa Singano, mchezaji huyo alielezwa apeleke mkataba halisi unaoonesha kuwa mkataba wake unaisha mwaka huu lakini matokeo yake akapeleka nakala. Nyange alionesha kwa mwandishi wa habari hii utofauti wa mkataba wa miaka mitatu aliosajiliwa kwa Sh milioni 13 na ule wa miaka miwili.
“Kitendo cha kudanganya umma kuwa mkataba wake umekwisha wakati ushahidi tunao, kitamgharimu kwasababu ukweli alisaini mbele ya mwanasheria kwa hiyo tunaweza kumshtaki kwa Mwanasheria kisha akashtakiwa Mahakamani,”alisema.
Alizungumzia kuhusu mshahara wa mchezaji huyo Kaburi alisema walikuwa wanamlipa Sh 700,000 kwa mwezi na kwasababu waliona kuwa mkataba wake unamalizika mwakani hivyo kuanzia Desemba mwaka huu angeanza kufanya mazungumzo na timu nyingine, lakini walitaka wamuongezee ufike Sh 800,000 na kuboresha mkataba wake.
Pia, alisema kuhusu nyumba walikubaliana katika mkataba alipwe Sh 600,000 lakini kwa vile alikuwa akiishi nyumbani kwao, wakakubaliana wampe gari aina ya Vits badala ya nyumba.
Alisema mchezaji huyo ameichafua klabu kwani inaleta picha mbaya hata kwa wachezaji wengine hivyo wanaweza kumchukulia hatua kuwa fundisho kwa wengine wanaotumia vyombo vya habari kupotosha.
Aidha habari kutoka ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinasema kuwa mkataba ilionao ni wa miaka mitatu.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker
Post a Comment