TANGAZO
6th June 2015
Wadau wa habari nchini wamepinga mpango wa serikali wa kupeleka miswada ya habari bungeni kama hati ya dharura na kutaka kusitishwa kwa zoezi hilo.
Wiki hii bunge lilielezwa kujadiliwa kwa miswada mbalimbali ikiwemo miswada miwili ya Haki ya kupata Habari na Huduma za Vyombo vya habari ambayo ilielezwa imepelekwa kama hati ya dharura lakini hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema ilipokelewa kama miswada na sio hati ya dharura.
Akisoma tamko hilo jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wadau wa Habari, Kajubi Mukajanga, alisema hawaoni sababu ya uharakishwaji wa miswada hiyo miwili wakati hawajapatiwa fursa ya kuipitia.
Alisema wadau hawajashirikishwa kuipitia, kuisoma, kuichambua na kutoa maoni yao.
Mukajanga alisema serikali itumie Mkutano wa 19 wa Bunge kusomwa miswada hiyo kwa mara ya kwanza kama hatua ya kuitayarisha kupokea maoni ya wadau kwa miezi inayokuja.
Alisema Bunge na uongozi wake lisikubali kupokea na kujadili miswada hiyo kwa utaratibu wa hati ya dharura.
“Kwa kuwa haki ya kupata habari ni haki wezeshi, hakuna budi kuhakikisha kunakuwapo na ushiriki mpana wa wananchi katika hatua zote za utungaji wa sheria hizi mbili,” Alisema.
Alisema serikali inatakiwa kuwezesha upatikanaji wa nakala za kutosha za miswada hiyo kwa umma na kutoa muda wa kutosha kwa wananchi kuchangia maoni yao kikamilifu.
Mukajanga alisema kinachotakiwa kufanyika ni serikali kufuata taratibu zinazotumika za uwasilishwaji na upitishaji wa miswada bungeni.
Alisema kitendo cha miswada hiyo kupelekwa bungeni kama hati ya dharura inaonyesha dhahiri kuwa serikali haikuwa na dhamira ya upatikanaji wa sheria hizo.
“Tunatarajia bunge litafanyakazi yake ya kuishauri serikali kufuata utaratibu mzuri wa uwasilishaji wa miswada hii na kuchangia miswada hiyo kwa kuzingatia maslahi mapana ya kimataifa wakati muafaka utakapofika,” alisema.
Alisema wakiwa kama wadau muhimu walilifanyia kazi suala hilo la upatikanaji wa Sheria ya Haki ya kupata Habari na Huduma za vyombo vya habari kwa taribani muongo mmoja wameshangazwa na usiri mkubwa uliopo katika kupelekwa miswada hiyo bungeni.
Mukajanga alisema wanatarajia kuwa mchakato huo wa kutunga sheria hizi mbili ungefanyika kwa uwazi matokeo yake umefanyiki kisiri.
Aidha, alisema wadau walipata taarifa kupitia ratiba ya mkutano wa 19 wa bunge bila kujulishwa wala kushirikishwa katika hatua za mwisho za matayarisho ya miswada hiyo.
Alisema taarifa ya kupelekwa kwa muswada hutolewa siku 21 kabla ya kusomwa bungeni lakini suala hilo halikufanyika.
Mwenyekiti Kituo cha Habari kwa Wananchi (TCIB), Deus Kibamba, alisema wadau wamekuwa wakishiriki wakati wote katika upatikanaji wa sheria hiyo, hivyo walitegemea kutakuwa na ushirikishwaji katika miswada hiyo.
Alisema kuna haja ya kufuatwa kwa utaratibu za uwasilishwaji wa miswada kwani kwa mara ya kwanza husomwa na kurudishwa kwa wadau ili waweze kuchangia maoni yao lakini kinachotaka kufanyika ni tofauti.
Alisema serikali isipoitoa miswada hiyo waliyoifanya kama hati ya dharura wataandaa tamko lao kama wadau.
CHANZO: NIPASHE
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker
Post a Comment