} });
 

TANGAZO

IDADI ya wagombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inazidi kuongezeka na jana wagombea wengine sita walichukua fomu na kufanya idadi ya watu wanaowania kumrithi Rais Jakaya Kikwete kufikia 10.
Hadi jana jioni, wanachama 10 wa chama hicho tawala walikuwa wamechukua fomu kuomba uteuzi wa kuwania Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kutokana na kasi hiyo kuna habari kuwa makada takribani 30 wamedhamiria kuchukua fomu kugombea urais kwa tiketi ya CCM idadi ambayo ni kubwa kuzidi ile ya mwaka 1995 ambako makada takribani 17 walijitokeza kugombea urais kupitia CCM.
Mwaka 2005 makada wa CCM ambao walijitokeza kuwania nafasi hiyo walikuwa ni 11. Kati ya hao, wanne walichukua fomu juzi na sita walichukua jana kwenye Makao Makuu ya CCM, Barabara ya Nyerere mjini hapa.
Hao ni Profesa Mark Mwandosya, Stephen Wassira, Balozi Amina Salum Ali na Charles Makongoro Nyerere waliochukua fomu juzi.
Waliochukua jana ni Katibu Msaidizi wa CCM wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa katika Ofisi Ndogo, Dar es Salaam, Amos Siyantemi, Waziri Mkuu wa zamani Frederick Sumaye, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal na Balozi mstaafu Ali Karume. Wengine ni Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
Wakati akikabidhi fomu kwa Dk Magufuli saa 11:30 jioni, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Oganaizesheni, Dk Muhammed Seif Khatib aliwaonya wagombea hao kuwa wakati wa kampeni bado.
“Hili sikuwaambia wenzako, lakini tutawaeleza, huu ni wakati wa kutafuta wadhamini, sio wakati wa kampeni. Hamuendi kutafuta kura, zingatieni hilo,” Dk Khatib alimueleza Dk Magufuli baada ya kumkabidhi fomu.
Naye Dk Magufuli ambaye alikuwa wa mwisho kukabidhiwa fomu jana, tofauti na wenzake tisa waliotangulia, hakuzungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa NEC katika makao makuu hayo.
Badala yake akiwa katika ukumbi huo wa kuchukulia fomu, Dk Magufuli ambaye hakutangaza nia kama wenzake badala yake akaibukia katika uchukuaji fomu, alisema anaomba kwanza akasome fomu alizopewa.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijali kufika hapa, lakini nashukuru pia kwa kupata document (hati) hii. Sijaisoma na wala masharti yake siyajui,” alisema Dk Magufuli ambaye pia ni Mbunge wa Chato mkoani Geita.
Akizungumza na waandishi wa habari alipochukua fomu, Siyantemi alisema anayo nia ya kugombea, sababu, sifa za mgombea urais na sifa za urais na uwezo wa kuongoza Taifa kwa kushirikiana na Watanzania wote anazo.
Alisema akichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania atazingatia kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa; kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi na kurejesha imani na matumaini ya wananchi kwa Serikali ya CCM.
Dk Bilal ambaye kama Dk Magufuli hawakutangaza nia kabla, alisema kaulimbiu yake ni ‘Mabadiliko ndani ya Umoja’ na kuwa amejitosa baada ya kutafakari maoni ya watu waliomshauri afikirie kuomba nafasi hiyo.
Alisema akiwa msaidizi wa karibu wa Rais Kikwete, alisema vipaumbele vyake ni kulinda msingi ya Utaifa, ushirikishwaji wa wananchi kiuchumi, matumizi mazuri ya rasilimali, kurejesha na kusimamia maadili na miiko ya uongozi pamoja na utumishi wa umma na kulinda haki za binadamu ikiwa ni pamoja na utawala bora.
Lowassa akifuatana na mkewe Regina, alikuwa wa tano kuchukua fomu jana saa 10:30 jioni na alisindikizwa na mamia ya watu na baadaye kutembea kwa miguu kwenda kusaka wadhamini katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Dodoma iliyoko karibu na Makao Makuu.
Akijibu swali kuhusu kuelekezewa shutuma na baadhi ya wenzake waliotia nia, Lowassa ambaye alitamba kuwa hana mpango wa kushindwa, alisema: “Mtu anayejiamini kwa hoja hazungumzii wengine, nachoka na tuhuma na matusi. Ingefaa watu wazungumzie rekodi zao wamefanya nini, rekodi ya kazi zao badala ya kutukanana, hizi ni siasa za majitaka".
Katibu wa NEC wa Oganaizesheni, Dk Khatib alisema uchukuaji fomu huo hauna Jumamosi wala Jumapili na kuwa leo watachukua fomu wanachama watatu.
Wa kwanza atakuwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Uchukuzi Samuel Sitta na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani.
Kinana atoa ya moyoni
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana ameasa wanachama wa chama hicho kuepuka kuongozwa na ushabiki katika kuchagua mgombea wa urais badala yake, wawe makini kupitisha mgombea anayefaa kwa kuzingatia vigezo vyote.
Kinana ambaye pia amesema utitiri wa wagombea nafasi hiyo usiwatie shaka wana CCM na akafafanua kuwa wanaojinadi siyo bidhaa, bali ni watu wanaotaka uongozi mkubwa katika nchi hivyo panahitajika uangalifu katika kuwapata.
“Nawasihi wana CCM msiongozwe na ushabiki ongozweni na hoja. Sio ushabiki. Viongozi wanaojinadi siyo bidhaa, hawa ni viongozi wanaotaka uongozi mkubwa sana wa nchi hii ,wekeni ushabiki kando tumieni busara, tumieni akili amueni mkiwa mmetulia,” alisema Kinana.
Kiongozi huyo wa juu wa chama alitoa wosia huo jana mjini Morogoro, alipokuwa akisalimiana na wana CCM akiwa safarini kwenda mkoani Kagera kwa ajili ya ziara ya siku 28 katika mkoa huo pamoja na Geita na Mwanza.
Kinana ambaye alikuwa akishangiliwa na wanachama waliokusanyika kumsalimia, alisema uwepo wa wagombea wengi wa nafasi hiyo ni haki ya wahusika kufanya hivyo na wanachama wawasikilize na kuwafanyia tathmini na baadaye apatikane anayefaa kuongoza nchi.
Imeandikwa na Stella Nyemenohi, Morogoro na Mgaya Kingoba, Dodoma

soma habar kilasiku kazi ya mikono yangu ni kuhakikisha unapata unachotaka +255 769 859 030 #ZAMU YAKO 2016

TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker

Post a Comment

 
Top