TANGAZO
WAKATI Watanzania na hasa viongozi wa sekta binafsi, wakijiandaa kupima uwezo na uelewa wa watangaza nia wa CCM, katika masuala muhimu ya kiuchumi kwenye mdahalo ulioandaliwa kesho kutwa, chama hicho kimepiga marufuku watangaza nia hao kushiriki midahalo hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho mjini hapa jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wa Oganaizesheni, Dk Muhammed Seif Khatib, amesema chama hicho hakiruhusu midahalo kwa makada wake hao kwa kuwa hakina mgombea mpaka sasa.
“Nasikia kuna midahalo lakini CCM hairuhusu wanaotaka urais kushiriki kwa sababu hadi sasa wao ni wagombea tu,” alisema Dk Khatib. “Kushiriki midahalo sasa ni kuchanganya wanachama, kulumbana na kupakana matope. Wagombea hao waache kushiriki midahalo.
“Na hao wanaoandaa midahalo wawasiliane na Makao Makuu kwa sababu kwa sasa hatuna muda mrefu, zimebaki wiki nne tu kwa ajili ya Mkutano Mkuu,” alisema.
Maandalizi
Kabla ya tamko hilo la CCM, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya CEO Round Table Tanzania (CEOrt), Ali Mufuruki alitangaza jana asubuhi kuwa mdahalo huo umeandaliwa na tayari baadhi ya watangaza nia wameshathibitisha kushiriki.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, watangaza nia waliokuwa wamethibitisha kushiriki ni watano na mdahalo huo ulikuwa ufanyike mara tatu, mara ya pili ukihusisha watangaza nia wa vyama vya upinzani na mara ya tatu watangaza nia wengine kutoka CCM.
Watangaza nia hao ambao kutokana na tamko la Dk Khatib wamezuiwa kuonesha uwezo wao kwa Watanzania, ni aliyekuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye na mmoja wa wanadiplomasia wakubwa, Balozi Amina Salum Ali ambaye ni mwanamke pekee hadi sasa aliyejitokeza kutangaza nia na kuchukua fomu ya kugombea urais.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigu- lu Nchemba.
Mufuruki alisema, mbali na uthibitisho kutolewa na watangaza nia hao, lakini washiriki kutoka sekta binafsi waliotakiwa kulipia Sh 100,000 ya kiingilio, walishaanza kulipia na akahadharisha kuwa ambao wangechelewa huenda wasingepata nafasi, kwa kuwa ukumbi wa mjadala unachukua watu wasiozidi 300.
Mdahalo huo ulitarajiwa kurushwa moja kwa moja na televisheni mbalimbali nchini kwa saa mbili kuanzi saa mbili asubuhi siku ya Jumatatu ijayo, ambapo wagombea walikuwa waulizwe maswali na jopo la wataalamu wa uchumi na masuala ya utawala bora.
Maeneo waliyotakiwa kuzungumzia ambayo pia maswali yangetoka huko, ni pamoja na kipaumbele chao cha uchumi katika kipindi cha mwaka 2015 mpaka 2020.
Pili wanatarajiwa kuzungumzia mikakati yao katika jitihada za kuhakikisha kunakuwepo utawala bora na kushinda vita dhidi ya rushwa.
Tatu, walitarajiwa wazungumze kuhusu malengo yao ya muda mrefu yatakayoleta maendeleo na kutunza utajiri wa maliasili wa Tanzania.
Pia walitarajiwa watoe maoni yao kuhusu dira zao, mikakati na jitihada za kuipeleka Tanzania katika mambo muhimu yatakayoharakisha uchumi wa muda mrefu.
Utetezi hatua ya CCM Dk Khatib alisema kuruhusu wanachama hao kushiriki midahalo sasa ni kuruhusu malumbano, kuvuruga wanachama wenzao na kutukanana.
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa kwa sasa CCM haina mgombea wa urais, hivyo haitakuwa vyema kwa wanachama hao wanaoomba uteuzi kuanza kushiriki midahalo.
Kampeni marufuku
Aidha, alisisitiza kauli yake ya juzi kuwa wanaochukua fomu wanatakiwa kwenda kusaka wadhamini mikoani na siyo kuendesha kampeni au kuomba kura.
“Wanakwenda kuomba wadhamini siyo kampeni. Kampeni hazijaanza, wajihadhari na hilo kwa sababu kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha kanuni na taratibu za chama,” alionya.
Alisema huu si muda wa kwenda na mabango na picha katika kusaka wadhamini, kwani mikoa na wilaya imeelekezwa kutenga eneo maalumu tu kwa ajili ya waliochukua fomu kudhaminiwa na wenzao.
“Mabango na picha pia haziruhusiwi, huu sio muda wa kampeni. Na hakuna mgombea hata mmoja atakayekosa mdhamini,” alisema Katibu huyo wa Oganaizesheni.
Wachukua fomu 13
Kuhusu uchukuaji fomu, alisema wamefikia wana CCM 13 baada ya watatu kuchukua hadi kufikia jana mchana. Waliochukua jana ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Uchukuzi Samuel Sitta na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani.
Wanachama wengine 10 walichukua kuanzia Jumatano ambayo ilikuwa siku ya kwanza na wengine juzi. Kwa idadi hiyo, CCM hadi sasa imevuna Sh milioni 13 kwani kila fomu ya urais inagharimu Sh milioni moja.
Hao ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira, Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Marekani, Amina Salum Ali na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere ambaye ni mtoto wa Mwalimu Nyerere.
Pia Katibu Msaidizi wa Idara ya Siasa na Ushirikiano wa Kimataifa (SUKI) wa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mawaziri wakuu wa zamani Frederick Sumaye na Edward Lowassa, Makamu wa Rais Dk Mohammed Gharib Bilal, Balozi mstaafu Ali Abeid Karume - mtoto wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume na Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli.
Watakaochukua leo Kwa mujibu wa Dk Khatib, leo watachukua fomu wanachama wawili; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Mussa Godwin Mwapango.
Aliwahimiza wanachama wengine wenye nia kufanya mawasiliano na ofisi yake, ili wapangiwe siku za kuchukua fomu kwani wanataka kumaliza kazi hiyo na kuendelea na shughuli nyingine za kichama.
Waliokwisha kutangaza nia ambao hawajachukua fomu ni Waziri Mkuu Miz- engo Pinda, Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba, wabunge William Ngeleja (Sengerema), Dk Hamis Kigwangalla (Nzega) na Luhaga Mpina (Kisesa).
Awali, Profesa Muhongo alikuwa wa kwanza kuchukua fomu jana na hakuzungumza na waandishi wa habari, badala yake alizungumza kwa ufupi baada ya kupewa fomu.
Mbunge huyo wa Kuteuliwa alisema hana woga na anajivunia uzoefu wake wa kitaifa na kimataifa katika kutumikia wananchi na kuongeza kuwa anawania nafasi hiyo akiahidi kujenga uchumi imara.
Sitta atumia basi
Naye Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, akifuatana na mkewe Margaret Sitta na wabunge kadhaa, aliingia katika viwanja vya CCM kwa basi aina ya Yutong atakalolitumia kusaka wadhamini.
Licha ya kusisitiza vipaumbele vyake alivyovitaja wakati wa kutangaza nia, alisema hatakuwa na kinyongo kama CCM itaamua kuwa safari hii Rais wa Tanzania atokea upande wa pili wa Muungano, Tanzania Zanzibar.
“Wote tuna haki sawa, hakuna ubaguzi. Binafsi akiteuliwa mgombea anayetoka Zanzibar nitalipokea kwa mikono miwili kwani kama nilivyoeleza mimi nataka kuongoza kwa miaka mitano tu, sigombei ili kuchuma tamaa,” alisema Sitta.
Akijibu swali jingine kuhusu kusakamwa kwa jinsi alivyoliendesha Bunge Maalumu la Katiba akiwa Mwenyekiti, mwanasiasa huyo mkongwe alisema ilikuwa ni ajenda na vita ya kiitikadi dhidi yake.
Alifafanua kuwa alichukiwa kwa sababu alizuia kuanzishwa kwa Serikali Tatu ambazo zilikuwa na nia ya kuvunja Muungano iliyokuwa ikitakiwa na CUF na pia kuanzisha Tanganyika na kuanzisha serikali ya majimbo manane nchini, iliyokuwa ikitakiwa na Chadema.
“Kwa hiyo hawa wenzetu, CUF na Chadema walikuwa na hayo mambo yao. Lakini nawahakikishia mimi ni imara, nina uwezo, uzoefu na ni mkweli.
Nipeni miaka mitano nchi niwape nchi iliyotulia na inayokwenda vizuri,” alijinasibu Sitta aliyewahi pia kuwa Spika wa Bunge katika Bunge la Tisa la Tanzania.
Akifunga dimba jana, Dk Kamani alisema amejipima na kuona anao uwezo wa kuiongoza Tanzania. “Mimi siombi urais kupitia CCM, naomba nikiwa ndani ya CCM.
Mimi pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Simiyu, watu wananiona ni mwanasiasa mgeni, lakini hakuna mahali urais unasomewa. Nina hakika nikipewa nafasi hii nitafanya vizuri,” alisema Dk Kamani ambaye pia ni Mbunge wa Busega.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker
Post a Comment