TANGAZO
| Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha. |
Malumbano
kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliotangazwa kufutwa na
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha,
yamezidi kushika kasi baada ya Waziri katika Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar (SMZ) kumshukia Maalim Seif huku akisisitiza kuwa ni lazima
uchaguzi urudiwe.
Jecha alitangaza kuufuta uchaguzi huo siku ya tatu baada ya
kufanyika Oktoba 25, kutokana na kile alichodai kuwa ulijawa na kasoro
nyingi na kwamba ‘haukuwa huru na wa haki’.
Hata hivyo, mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (Cuf),
Maalim Seif Shariff Hamad, amepinga kufutwa kwa uchaguzi huo aliodai
alikuwa akielekea kushinda kwa asilimia 52.87 kutokana na karatasi za
matokeo waliyopata kutoka katika vituo vyote vya kupigia kura huku CCM
waliomsimamisha Dk. Ali Mohamed Shein, kutetea nafasi yake wakiunga
mkono uamuzi wa Jecha. Jumla ya vyama nane vilivyoshiriki uchaguzi huo
vinapinga kurudiwa kwake.
‘Wanaosema kuwa uchaguzi urejewe waachieni wenyewe. Sisi katika CUF
hakuna msamiati huo kwa sasa. Kurejea uchaguzi huo siyo msimamo wetu,’
Maalim Seif alisema juzi kuwaambia wafuasi wa chama chake.
Kadhalika, waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje wametaka
majumuisho ya kura ya uchaguzi huo uliosaidia kupatikana kwa matokeo ya
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyomuwezesha Dk. John
Magufuli wa CCM kushinda yaendelee kwani ulikuwa huru na wa haki na
hakuna sababu za msingi kuufuta. Baadhi ya waangalizi hao ni wa kutoka
Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Ulaya (EU), Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),
Jumuiya ya Madola na pia balozi za nchi kama Uingereza, Marekani na
Ireland ya Kaskazini zimeisihi ZEC kuendelea na mchakato wa uchaguzi huo
kwani hakukuwa na kasoro kubwa kiasi cha kuufuta.
Hata hivyo, Msemaji wa SMZ, ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, amesema uchaguzi huo ni lazima
urudiwe kwani ‘haukuwa huru na wa haki’ kama alivyosema Jecha na pia
kupongeza uamuzi huo aliodai umeihakikishia amani na utulivu Zanzibar
hasa baada ya Maalim Seif kuibuka na kuonyesha kuwa ni yeye ndiye
aliyeshinda.
Waziri Abodu alisema kinachosubiriwa sasa ni ZEC kutangaza tarehe
ya kufanyika kwa uchaguzi huo na hivyo ni vyema vyama vyote vikatambua
jambo hilo.
‘Uchaguzi lazima ufanyike Zanzibar, wananchi wapate haki yao
kidemokrasia ya kuchagua viongozi wanaowataka baada ya uchaguzi wa
mwanzo kuvurugika.îalisema Aboud.
‘Aliongeza kuwa alichofanya Jecha ni sahihi kwani alitumia burasa
na hekima kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu ili kulinda amani na Umoja wa
Kitaifa na hadi sasa, uamuzi huo umesaidia kuivusha Zanzibar ikiwa
katika hali ya amani baada ya uchaguzi.
‘Mwenyekiti alitumia busara na hekima kufuta matokeo ya uchaguzi.
Bila ya hivyo, Zanzibar ilikuwa katika hatari ya kumwagika damu,’
alisema Aboud na kuongeza:
‘Kitendo cha mgombea wa CUF kujitangaza mshindi kabla ya matokeo ya
tume kulisababisha hali ya kisiasa kuchafuka. Bila ya busara na hekima
za mwenyekiti (Jecha) leo amani isingekuwapo Zanzibar,’ alisema Aboud.
Aboud alisema licha ya Maalim Seif kujitangazia ushindi, pia
uchaguzi wa Oktoba 25 ulitawaliwa na vitendo vya udanganyifu ikiwamo
idadi ya wapigakura kuwa kubwa kuliko orodha ya wapigakura katika vituo.
Kadhalika, alisema kitendo cha mgombea Maalim Seif kujitangaza
mshindi kilichangia kuvuruga uchaguzi huo hasa baada ya maafisa wa ZEC
kujikuta wakigawanyika na hivyo uamuzi wa kuufuta ulikuwa sahihi.
HAKUNA KAMPENI
Katika hatua nyingine, Aboud alisema uchaguzi huo utakaorudiwa
baada ya ZEC kutangaza ratiba hautakuwa na kampeni kwa sababu kila chama
kimefanya kampeni za kutosha; lakini wananchi watapewa elimu ya uraia
ili kuhakikisha kuwa wanajitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa marejeo.
Aidha, alisema watendaji wote wa ZEC au mamlaka yoyote, ambao
watabainika kuhusika na kuvuruga uchaguzi wa Oktoba 25 watachukuliwa
hatua za kisheria na uchunguzi mzito umeshaanza kufanyika kabla ya watu
hao kukamatwa.
Mkurugenzi wa zec, Salum Kassim Ali, alisema jana kuwa bado
hawafahamu ratiba ya kufanyika kwa uchaguzi huo, lakini alisema wakati
ukifika wananchi watajulishwa.
Vyama vinane kati ya 14 vilivyokuwa vimesimamisha wagombea
vinapinga kurudiwa kwa uchaguzi huo, wakidai ulikuwa ‘huru na wa haki’
na kwamba, hakuna kifungu kinachompa Jecha mamlaka ya kufuta uchaguzi
huo.
Mbali na CUF, vyama vingine vinavyopinga kurudiwa uchaguzi ni DP,
Chauma, NRA, Demokrasia Makini, Jahazi Asilia, SAU na ACT- Wazalendo.
Aidha, vyama vingine mbali na CCM vinavyounga mkono kufutwa
uchaguzi huo ni CCM, CCK, TLP na AFP. Chama cha Tadea ambacho pia
kilishiriki uchaguzi huo bado hakijatoa msimamo wake.
TUME HAKI ZA BINADAMU, ACT
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Tom
Nyaduga, amesema Jecha hakuwa na nguvu za kikatiba na kisheria za kufuta
matokeo ya uchaguzi huo Oktoba 28 mwaka huu na hivyo haoni sababu ya
kurudiwa kwa uchaguzi huo.
Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ramadhani Suleiman
Ramadhan, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana akipinga pia kufutwa
kwa uchaguzi huo.
Alisema hakuna sababu ya kuufuta uchaguzi huo kwa vile ulikuwa huru
na wa haki katika hatua zake zote kwa mujibu wa viwango vya kitaifa na
kimataifa kama ilivyothibitishwa na waangalizi wa uchaguzi wa ndani na
nje.
Pia ACT wametoa salamu za pongezi kwa Rais, Dk. John Magufuli na
makamu wake, Samia Suluhu Hassan kwa kushinda uchaguzi na kuapishwa
kushika nyadhifa hizo.
CHANZO:
NIPASHE
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by TeachMaker
Post a Comment